Tuesday, May 8, 2012

Mfumo Mpya wa Sheria za Ardhi



Waashiki wa sheria watakubaliana nami kuwa mfumo wa sheria umebadilika kufuatana na kupitishwa sheria mpya za ardhi.
Rais aliziidhinisha miswada hii na kuzifanya kuwa sheria tarehe 27 Aprili 2012:

v  Land Act (No. 6 of 2012);

v  The Land Registration Act (No. 3 of 2012); na

v  The National Land Commission Act (No. 5 of 2012).

Sheria za ardhi ambazo zilikuwa zikitumika hapo awali zilikuwa:

v    The Registered Lands Act (RLA);

v    The Registration of Documents Act (RDA);

v    The Governments Lands Act (GLA);

v    The Indian Transfer of Property Act (ITPA);

v    The Land Titles Act (LTA);

v    The Registration of Titles Act


Baadhi za lawama ambazo zimekuwa zikilimbikiziwa sheria za ardhi za hapo awali ni kuwa zilikuwa zimezagaa hivi kwamba aliyetaka kuzichunguza angetatizika. Wanasheria na mawakili ambao walifaa kutumia fomu na kuandika mikataba ya ardhi hawakufurahia hali hiyo. Hivyo basi, sheria hizi mpya ni jambo zuri.

Katika makala yatakayofuata, nitaangazia baadhi za kasoro za sheria hizi mpya na kutoa ulinganisho na mifumo ya hapo awali.

Thursday, May 3, 2012

MARAFIKI WA VITABU

Itanibidi nihifadhi blogu ambayo nimegundua leo hapa ili nisiisahau.

Hii blogu ina taarifa nzuri kwa wale wanaopenda vitabu.

Link yake ni Marafiki wa Vitabu.

Asante.

Friday, April 20, 2012

Elewa Katiba Yako: Makala ya Kwanza



Baada ya kusomea taaluma ya Sheria kwa muda mrefu, inanipasa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya sheria ambayo yanawatatanisha ama hawajapata fursa ya kuzisoma. Mwanzo, mtaniruhusu kudurusu vipengele muhimu yanayohusu bunge. Kuelewa bunge ndiko kuelewa jinsi ambavyo inaendesha masuala yake na matarajio yako mwananchi kwa wajibu unaomkabidhi kwa kumchagua.

Imenibidi kuwasilisha ujumbe huu kwa Kiswahili kwa sababu lugha ya mkoloni si wengi wanaizungumza na kuielewa. Pia, elimu kwa umma inapaswa kuwa kwa lugha inayoeleweka kwa urahisi.

Muhtasari:

Katiba ya Jamhuri ya Kenya inazungumzia suala la Bunge katika Sura ya nane kuanzia kipengee cha 93 hadi 128. Imegawanywa katika sehemu sita.

Sehemu mbali mbali

Sehemu ya Kwanza— Kuundwa na jukumu la Bunge
Sehemu ya Pili— Wanachama wa Bunge
Sehemu ya Tatu—  Maafisa wa Bunge
Sehemu ya Nne— Taratibu za kupitisha sheria
Sehemu ya Tano—Taratibu na sheria za Bunge
Sehemu ya Sita- Ziada

Haya basi twende moja kwa moja hadi Sura ya Nane.

~

SURA YA NANE
BUNGE

Kuundwa kwa Bunge
93.     (1) Kuna Bunge buniwa la Kenya litakalojumuisha Bunge na Seneti.
          (2) Bunge na Seneti zitatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba hii.


Jukumu la Bunge
94.    (1) Jukumu la kutunga sheria la Jamhuri hii katika kiwango cha kitaifa ni la             Bunge.
(2) Bunge hutokeza tofauti za kitamaduni katika taifa, linawakilisha maoni ya
watu na hutekeleza mamlaka yake.
……

Jukumu la Bunge
95.     (1) Bunge linawakilisha watu wa maeneo bunge na matakwa muhimu katika Bunge.
          (2) Bunge lina uwezo wa kupitisha sheria kulingana na sehemu ya 4 katika sura hii.
          (4) Bunge lina jukumu la—
(a)   kuidhinisha kugawana kwa mapato miongoni mwa viwango    mbalimbali vya  serikali na miongoni mwa serikali zenyewe katika kila kiwango na kukadiria hazina ya gharama ya serikali ya kitaifa na taasisi nyingine za Serikali ya kitaifa kwa mujibu wa Sura ya Kumi na Mbili;
(b) kutenga fedha za matumizi za serikali ya Kitaifa na sasi zingine za Taifa;
 (c) kufuatilia kuona iwapo kumekuwa uwazi katika matumizi ya rasilmali za kitaifa.
          (5) Bunge lina jukumu la—
(a) kuchunguza utendakazi wa ofisi ya Rais, Naibu wa Rais na maofisa wa Serikali na ikiwezekana kuanzisha hatua za kuwatoa ofisini; na
(b) kuchunguza kwa makini na kusimamia hatua zinazochukuliwa na taasisi za Serikali.
(6) Bunge lina mamlaka ya kuidhinisha matangazo ya vita na kuendelezwa kwa tangazo la muda wa hali ya hatari.

Jukumu la Seneti
96.  (1) Seneti linawakilisha kaunti, na litashughulikia masuala ya kaunti za serikali zao.
      (2) Seneti litashiriki katika kukusanya na kutunga sheria ya kitaifa na kulinda maslahi ya        serikali hiyo iliyogatuliwa kwa mujibu wa vipengee vya 109 hadi 113.
    (3) Seneti litashughulika na kutenga fedha za matumizi za serikali ya Kitaifa katika serikali iliyogatuliwa kwa mujibu wa kipengee cha 217, na kuchunguza kwa makini matumizi za pesa za serikali.
   (4) Seneti litajishirikisha  katika uchunguzi wa makini wa Maafisa wa Serikali, kuchunguza utendakazi wa ofisi ya Rais au Naibu wa Rais na ikiwezekana kuanzisha hatua za kuwatoa ofisini kwa mujibu wa kipengee cha 145.

~
Itabidi nikome hapo kwa leo. Katika makala mengine, nitatathmini vipengele vingine vilivyomo ndani ya Katiba.

Nikisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Jumuiya ya Tanzania, nimefurahishwa na jinsi ambavyo wametumia lugha ya Kiswahili haswa katika haya:

     i.        Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii neno "…." Maana yake ni….
   ii.        Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1),….
 iii.        Ibara kwa kiingereza ni Section.
  iv.        Misingi ya Katiba kwa kiingereza ni Preamble.

Thursday, April 19, 2012

Nimerudi


Wasomaji wangu,

Kwanza lazima nitoe msamaha wangu wa dhati kwa kutulia kwa kipindi cha muda mrefu. Nimerudi kwa kishindo na nimeandaa makala muhimu ambayo yanaelezea baadhi ya mambo ambayo ninayaona kuwa muhimu.

Tegea makala yangu baada ya muda mfupi.

Wasaalam,
Lorot 

Friday, March 18, 2011

Tafakari za Lorot Mwana wa Milima


"Maisha yatakupa maji vuguvugu.Maisha yatahitaji hekima yako na busara kutambua kuwa wakati mwingine wahitaji kugeuza maji ya kuoga yakawa ugali ama chai ama hata uji."-- Lorot Mwana wa Milima

Mgeni akaribishwa nyumbani. Kutokana na uhasama ambao unakithiri katika chumba hicho kati ya bwana na bibi, mgeni anajipata katikati ya vurugu hili. Anapoagizia maji ya kuoga na suala ambalo laibuka ni iwapo maji yenyewe yatakuwa baridi au moto, mwenzetu mgeni anaonelea yawe vuguvugu. Lakini anabadilisha nia kisha anapendekeza maji yenyewe (yaliyokusudiwa kuoga nayo) yapikiwe ugali. Mgeni amejihami na sufuria ( Wageni nao!).

Gesi linaisha hata kabla ugali haijapikwa. Lakini mgeni havunjiki moyo. Mgeni anauliza ikiwa maji yenyewe yalikuwa yamechemka . Kisha akiridhika na jibu kuwa maji yenyewe yalikuwa na moto kiasi, anaomba apikiwe uji!

Hili lilikuwa na suala katika kichekesho cha Churchill Live inayotazamwa na wengi wa Wakenya. Nakumbuka huyu mhusika jinsi alivyonichekesha na vitimbi vyake. Kweli Wakenya tuna vipaji!

Naam, suala hilo lilinielekeza kufikiria juu ya maisha yetu kama binadamu. Katika Kiingereza, wao husema "If life gives you a lemon, make a lemonade". Ikiwa maisha yatakupa limau, basi tengeneza sharubati ya limau. Maisha yatakupa vipengele kadha wa kadha ambavyo katika akili yako hutaweza kutarajia vinaweza kuwa daraja lako la kukufikisha ng'ambo ya pili ya ufanisi. Maisha yatakupa maji vuguvugu.Maisha yatahitaji hekima yako na busara kutambua kuwa wakati mwingine wahitaji kugeuza maji ya kuoga yakawa ugali ama chai ama hata uji.

Tafakari za Lorot Mwana wa Milima.

Thursday, March 17, 2011

Nasikitika kukujulisha Kuwa Huyo Kiongozi ni Mwizi!



















[Picha kutoka kwa toptipsfortrips.blogspot.com]

First they came for the communists, and I didn't speak out because I wasn't a communist. Then they  came for the trade unionists, and I didn't speak out because I wasn't a trade unionist. Then they came for the Jews, and I didn't speak out because I wasn't a Jew. Then they came for me and there was no one left to speak out for me- Pastor Martin Niemoller
Tafsiri:
Mwanzo waliwajia wakomunisti, nami sikuzungumza kwani sikuwa mkomunisti. Kisha wakawajia, nami sikuzungumza kwani sikuwa.Kisha wakawajia mayahudi, nami sikuzungumza kwani sikuwa myahudi. Kisha wakanijia mimi lakini hakukuwa wakunizungumzia kwani hakukuwa na yeyote. - Pastor Martin Niemoller


 Tuambiane ukweli: tunapowachagua viongozi wetu kisha tukasikika tukiguna kuwa hawatuwakilishi sisi katika maeneo bunge yetu au hata kutamka maneno yasiyoandamana na imani na misukumo yetu ni nani wa kulaumiwa zaidi kama si sisi? Je, ni nani mwenye akili mauzauza iwapo kiongozi huyu hataoa sera zetu na maendeleo tunayotaraji kutoka kwake? Iwapo kiongozi huyu tutamtazama katika runinga akituhimiza kusikiliza porojo zake zisizo msingi, ni nani wa kulaumiwa?


 Naam, wapo viongozi wanaojaribu kupalilia amani na maendeleo na kuirutubisha na semi zilizojaa heshima na falsafa zinazotupandisha ari ya kufanya vyema zaidi. Wapo viongozi ambao hulka zao pekee hazitowaruhusu kuipora mali yetu ya umma ili kujibinafsisha. Wapo viongozi ambao darahima si suala ambalo litawasukuma katika matamshi na matendo yao. La kuvunja moyo labda ni kwamba hawa viongozi ni adimu sana hapa nchini waweza kuzunguka Kenya nzima ukatamaushwa na uchache wao!

Wengi wa wanasiasa wetu wanahitaji maombi. Sikusudii kukushtua lakini ukifungulia runinga yako saa moja  jioni utasikiza vitimbi vyao visivyo na msingi. Cheche za matusi wataziamsha, vichekesho visivyo na msingi wa kuendeleza udugu watavisema, propaganda watazua alimradi katika mitazamo yao itawaongezea “political mileage” si hoja. Mola turehemu.

Vipengele katika katiba vitafanyiwa kazi chapwa kwa kuguna au kwa wasiwasi ya mwasi. Katika bunge letu, miswada haitapitishwa na kujadiliwa ipasavyo bali vita vya ndani kwa ndani ya kujijenga kisiasa au kuharibu mwenzio kisiasa vitakuwa vitu vya kawaida na ya kukubalika. Nje ya bunge, tutawasikia wakitueleza jinsi ambavyo mdahalo ulinoga ilhali tukiwatazama katika runinga walikuwa wamesinzia.

Na sisi? Na sisi je? Tutasalia na shida zetu tu tusiwe na wa kutuhimiza au kututimizia malengo. Katika giza na simanzi ya vyumba vyetu tutalalama tusiwe na wa kutuhamasisha. Katika giza la usiku kama huu, tutatapatapa bila mwelekeo tusijue jinsi ambavyo siku ya jua ya maendeleo na sera za kujenga zinavyopendeza. Tutakapofumaniwa na ushirikina wa umaskini na kifo cha ghafla kwa ajili ya dhiki zinazotuandama, hakuna atakayesikiza kelele zetu za mayowe. Kelele zetu zitabaki kelele zetu tu na kero kwa viongozi wetu tuliowachagua. Si ajabu katika majumba yao ya kifahari watamaka:

“Vilio vyao vya pesa nane si muhimu! Ikiwa wanadhani watanitisha wajitose basi katika bahari waliwe na papa na nyangumi! Sauti zao zinaudhi, ni kelele katika masikio yangu!”

Kuna nukuu moja ambalo linanihimiza mno. Linasema, “taifa hupata viongozi ambao linachagua”. A nation gets the leaders it chooses. Ikiwa taifa litachagua viongozi ambao wataendeleza maadili na sera yake, taifa hilo litaendelea. Ikiwa taifa litachagua viongozi ambao ni wabadhirifu, wanaopenda upyoro, wanaoweza fanya lolote ili kunyakua viti vya kisiasa na wafisadi waliopora taifa letu, taifa hili litazidi kusalia nyuma kimaendeleo. Jukumu hili ni letu. Tuwachague viongozi wanaotupeleka mbele na si vikaragosi ambao misingi yao maishani ni kukusanya mihela na kuchemua matusi!

Tuesday, October 12, 2010

Toba Za Lorot Mwana Wa Milima

Mabibi na Mabwana, wenzangu mnaonipenda na msionipenda,Wanamilima wote, nina toba. Samahani, tatu. Kumbukizi zangu zimenisakama. Nimezama katika bahari ya luja kwa takriban saa mia moja ishirini katika tafakari na tafakuri si haba. Akili zangu zaweza kuniduru. Timamu zangu zinanielemea. Naweza kujitia hamnazo kuwa sijihusishi lakini akili yangu haitaniruhusu.

Tuambiane ukweli, basi. Sitakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa.

Mosi, tumehadaiwa, tumedanganywa, tumetapeliwa. Uwongo tumelishwa, uwongo tusiouelewa bayana. Tumekuwa watu baki. Tumejitia hamnazo isiyo kifani. Mfano, katika lile somo la hesabu. Ulifunzwa kipengele Fulani kiitwacho inteja na namba laini. Pia, ukafunzwa ikwesheni zinazoenda sambamba ( walioenda shule watakuambia simultaneous equation). Mwalimu wako kisha akajitosa katika mambo yake ajabu ajabu kisha akakufunza concept moja kibao kinachoitwa Naotiko Mail (Nautical Miles). Na lugha moja ya wapiga ramli iitwayo matrix. Muungwana, tangu lini namba zikasimama moja juu ya nyingine ukadhani ghorofa halafu ukaiita hesabu? Makubwa haya! Dunia imepasuka mahali! Tuambiane ukweli.

Pili, kasheshe zangu zimenitia matatani. Ninapopiga soga za Milima, ninapokariri hadithi za Milima, ninapozifuma na kufumua na kuipinda na kuipindua, wengi hamnielewi. Mwazisoma tu kisha mnamaka Lorot Mwana wa Milima, haambiliki hasemeki. Hawezi akaaminika. Ni kinyonga.

Sikatai.

Nakiri mashtaka. Lakini kumbuka mwenzangu, mwana na binti wa Milima, kwamba dunia hii yetu ina kunga zake tusizozielewa. Imejipinda ajabu. Haiko laini. Lau ingekuwa laini ungenilimbikizia malalamishi yako, Muungwana. Ulimwengu ni malimwengu. Hivyo basi, ninapochukua jukumu la usanii na kuchora dira ya dunia jinsi ninavyotazama mie sifurahii hili jukumu. Linanipa jakamoyo, linanitia huzuni, majonzi na jitimai si haba. Mara si moja wakati nimejiambia kuwa nitaitupa michoro hii baharini ili iliwe na papa na nyangumi. Lakini, kwa kuponda kwa awali, ninajiambia mimi ni Msanii, nachora dunia jinsi ilivyo. Sizidishi sipunguzi. Waweza kuwa hakimu, mwana wa Adamu mwenzangu.

Lakini mimi, Lorot Mwana wa Milima, sitakuwa hakimu. Siwezi kukashifu, sitafoka, sitakaripia. Nilicho nacho ni riwaya na ngano za Milima. Zimezaliwa ndani ya mapango ya milima. Zimehifadhiwa na wanamilima kama wewe. Kinitiacho huzuni ni kwamba zimeoshwa na watu katika zumbukuku zao. Hata hivyo, mimi ni Mjumbe ninayewasilisha ujumbe kwa Wanamilima. Wanamilima wanaweza kunikashifu, kunizomea, kunifokea hata kuniua. Lakini haidhuru. Mirindimo na rungwaya za Milima zitaendelea kurindima na kupaaza sauti toka mlima mmoja hadi mwingine. Katika vikelele hivi, Lorot Mwana wa Milima, atazisikiza na kuziwasilisha jinsi zilivyo. Milima imempatia wadhifa na imani.

Tatu, na usikanganyike Mwana Milima mwenzangu: Salem Lorot Dick ( ndio hivyo tena na Majina ya Kizungu, sisemi kitu) na Lorot Mwana wa Milima ni watu tofauti kama alama nyekundu na kijani kibichi. Salem ni msiri, aliyesetiri kila kitu kilicho chake kifuani na hapendi kujitia katikati ya watu kama mchuzi katikati ya ugali. Salem amelogwa na shughuli zinazomwandama kibao. Kwa upande mwingine, Lorot Mwana wa Milima ni kinyume kabisa cha Salem. Lorot ni mcheshi, mwenye kasheshe, ni mfitini, anapenda umbeya, atakuambia mechi kati ya Iraki na Sofa Paka ilichezwa vipi mwaka wa 1981. Lorot Mwana wa Milima ana ngano si haba za Milima.

Hivyo basi, unapofura kama kaimati na kunihukumu kwamba Salem, wewe umevunja mwiko za wanamilima, huaminiki tena, umepoteza fahamu zako. Kisha, mie Lorot Mwana wa Milima nitajibu kwa Ungwana wa Wanamilima walionifunza utu na ubinadamu kuwa mimi nina heshima za Milima. Elekeza lawama kwa Lorot Mwana wa Milima, si mimi Salem. Na nikifikiria zaidi kuhusu mambo haya ninamwonea huruma Lorot Mwana wa Milima. Amesongwa na hadithi za kusononesha za Wanamilima. Uwendawazimu umesheheni kwenye milima. Anapotunga hadithi hizo basi ni mirindimo ya milima. Tutamlaumu vipi anayewasilisha ujumbe huu?

Kwa kumalizia, wanamilima, nimejieeleza bayana. Nafsi yangu imetulia. Tafakuri zangu zimenyooka. Iwapo kutakuwepo na tashwishi kuhusu nani aliyeendika ujumbe huu usichelee kusema Lorot Mwana wa Milima!

Asante Mwana Milima.