Tuesday, October 12, 2010

Toba Za Lorot Mwana Wa Milima

Mabibi na Mabwana, wenzangu mnaonipenda na msionipenda,Wanamilima wote, nina toba. Samahani, tatu. Kumbukizi zangu zimenisakama. Nimezama katika bahari ya luja kwa takriban saa mia moja ishirini katika tafakari na tafakuri si haba. Akili zangu zaweza kuniduru. Timamu zangu zinanielemea. Naweza kujitia hamnazo kuwa sijihusishi lakini akili yangu haitaniruhusu.

Tuambiane ukweli, basi. Sitakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa.

Mosi, tumehadaiwa, tumedanganywa, tumetapeliwa. Uwongo tumelishwa, uwongo tusiouelewa bayana. Tumekuwa watu baki. Tumejitia hamnazo isiyo kifani. Mfano, katika lile somo la hesabu. Ulifunzwa kipengele Fulani kiitwacho inteja na namba laini. Pia, ukafunzwa ikwesheni zinazoenda sambamba ( walioenda shule watakuambia simultaneous equation). Mwalimu wako kisha akajitosa katika mambo yake ajabu ajabu kisha akakufunza concept moja kibao kinachoitwa Naotiko Mail (Nautical Miles). Na lugha moja ya wapiga ramli iitwayo matrix. Muungwana, tangu lini namba zikasimama moja juu ya nyingine ukadhani ghorofa halafu ukaiita hesabu? Makubwa haya! Dunia imepasuka mahali! Tuambiane ukweli.

Pili, kasheshe zangu zimenitia matatani. Ninapopiga soga za Milima, ninapokariri hadithi za Milima, ninapozifuma na kufumua na kuipinda na kuipindua, wengi hamnielewi. Mwazisoma tu kisha mnamaka Lorot Mwana wa Milima, haambiliki hasemeki. Hawezi akaaminika. Ni kinyonga.

Sikatai.

Nakiri mashtaka. Lakini kumbuka mwenzangu, mwana na binti wa Milima, kwamba dunia hii yetu ina kunga zake tusizozielewa. Imejipinda ajabu. Haiko laini. Lau ingekuwa laini ungenilimbikizia malalamishi yako, Muungwana. Ulimwengu ni malimwengu. Hivyo basi, ninapochukua jukumu la usanii na kuchora dira ya dunia jinsi ninavyotazama mie sifurahii hili jukumu. Linanipa jakamoyo, linanitia huzuni, majonzi na jitimai si haba. Mara si moja wakati nimejiambia kuwa nitaitupa michoro hii baharini ili iliwe na papa na nyangumi. Lakini, kwa kuponda kwa awali, ninajiambia mimi ni Msanii, nachora dunia jinsi ilivyo. Sizidishi sipunguzi. Waweza kuwa hakimu, mwana wa Adamu mwenzangu.

Lakini mimi, Lorot Mwana wa Milima, sitakuwa hakimu. Siwezi kukashifu, sitafoka, sitakaripia. Nilicho nacho ni riwaya na ngano za Milima. Zimezaliwa ndani ya mapango ya milima. Zimehifadhiwa na wanamilima kama wewe. Kinitiacho huzuni ni kwamba zimeoshwa na watu katika zumbukuku zao. Hata hivyo, mimi ni Mjumbe ninayewasilisha ujumbe kwa Wanamilima. Wanamilima wanaweza kunikashifu, kunizomea, kunifokea hata kuniua. Lakini haidhuru. Mirindimo na rungwaya za Milima zitaendelea kurindima na kupaaza sauti toka mlima mmoja hadi mwingine. Katika vikelele hivi, Lorot Mwana wa Milima, atazisikiza na kuziwasilisha jinsi zilivyo. Milima imempatia wadhifa na imani.

Tatu, na usikanganyike Mwana Milima mwenzangu: Salem Lorot Dick ( ndio hivyo tena na Majina ya Kizungu, sisemi kitu) na Lorot Mwana wa Milima ni watu tofauti kama alama nyekundu na kijani kibichi. Salem ni msiri, aliyesetiri kila kitu kilicho chake kifuani na hapendi kujitia katikati ya watu kama mchuzi katikati ya ugali. Salem amelogwa na shughuli zinazomwandama kibao. Kwa upande mwingine, Lorot Mwana wa Milima ni kinyume kabisa cha Salem. Lorot ni mcheshi, mwenye kasheshe, ni mfitini, anapenda umbeya, atakuambia mechi kati ya Iraki na Sofa Paka ilichezwa vipi mwaka wa 1981. Lorot Mwana wa Milima ana ngano si haba za Milima.

Hivyo basi, unapofura kama kaimati na kunihukumu kwamba Salem, wewe umevunja mwiko za wanamilima, huaminiki tena, umepoteza fahamu zako. Kisha, mie Lorot Mwana wa Milima nitajibu kwa Ungwana wa Wanamilima walionifunza utu na ubinadamu kuwa mimi nina heshima za Milima. Elekeza lawama kwa Lorot Mwana wa Milima, si mimi Salem. Na nikifikiria zaidi kuhusu mambo haya ninamwonea huruma Lorot Mwana wa Milima. Amesongwa na hadithi za kusononesha za Wanamilima. Uwendawazimu umesheheni kwenye milima. Anapotunga hadithi hizo basi ni mirindimo ya milima. Tutamlaumu vipi anayewasilisha ujumbe huu?

Kwa kumalizia, wanamilima, nimejieeleza bayana. Nafsi yangu imetulia. Tafakuri zangu zimenyooka. Iwapo kutakuwepo na tashwishi kuhusu nani aliyeendika ujumbe huu usichelee kusema Lorot Mwana wa Milima!

Asante Mwana Milima.

No comments:

Post a Comment