"Maisha yatakupa maji vuguvugu.Maisha yatahitaji hekima yako na busara kutambua kuwa wakati mwingine wahitaji kugeuza maji ya kuoga yakawa ugali ama chai ama hata uji."-- Lorot Mwana wa Milima
Mgeni akaribishwa nyumbani. Kutokana na uhasama ambao unakithiri katika chumba hicho kati ya bwana na bibi, mgeni anajipata katikati ya vurugu hili. Anapoagizia maji ya kuoga na suala ambalo laibuka ni iwapo maji yenyewe yatakuwa baridi au moto, mwenzetu mgeni anaonelea yawe vuguvugu. Lakini anabadilisha nia kisha anapendekeza maji yenyewe (yaliyokusudiwa kuoga nayo) yapikiwe ugali. Mgeni amejihami na sufuria ( Wageni nao!).
Gesi linaisha hata kabla ugali haijapikwa. Lakini mgeni havunjiki moyo. Mgeni anauliza ikiwa maji yenyewe yalikuwa yamechemka . Kisha akiridhika na jibu kuwa maji yenyewe yalikuwa na moto kiasi, anaomba apikiwe uji!
Hili lilikuwa na suala katika kichekesho cha Churchill Live inayotazamwa na wengi wa Wakenya. Nakumbuka huyu mhusika jinsi alivyonichekesha na vitimbi vyake. Kweli Wakenya tuna vipaji!
Naam, suala hilo lilinielekeza kufikiria juu ya maisha yetu kama binadamu. Katika Kiingereza, wao husema "If life gives you a lemon, make a lemonade". Ikiwa maisha yatakupa limau, basi tengeneza sharubati ya limau. Maisha yatakupa vipengele kadha wa kadha ambavyo katika akili yako hutaweza kutarajia vinaweza kuwa daraja lako la kukufikisha ng'ambo ya pili ya ufanisi. Maisha yatakupa maji vuguvugu.Maisha yatahitaji hekima yako na busara kutambua kuwa wakati mwingine wahitaji kugeuza maji ya kuoga yakawa ugali ama chai ama hata uji.
Tafakari za Lorot Mwana wa Milima.
No comments:
Post a Comment