Tuesday, October 12, 2010

Zeruzeru: Hotuba ya Lorot Mwana wa Milima

Kisha nikasimama juu ya kilima kidogo, umati mkubwa umenizingira. Wapo waliokuwa wakilia, wengine wakijibiringisha kana kwamba wamepagawa. Nilikuwa na ujumbe. Na ujumbe huo ulikuwa na uzito wake ambao kidogo singeweza kuihimili.
Kisha nikaanza usemi wangu mimi Mwana wa Milima:
“Wanamilima, nina huzuni leo. Sina ucheshi. Bashasha imeniondoka na suduri yangu ni jakamoyo na simanzi. Habari hii ni juu ya ndugu zetu zeruzeru. Mila tunayo, desturi tunazo, itikadi tumezihifadhi lakini huu uhasama juu ya wenzetu zeruzeru si mila, desturi na itikadi za wanamilima. Kamwe, ukatili juu ya ndugu zetu haioani vyema na weupe wa nyoyo zetu.
“Anapozaliwa zeruzeru, huzaliwa sawa na watoto wengine. Naomba kukosolewa ikiwa sineni ukweli. Milio yao si za nyani ama hayawani. Wao hubebwa miezi tisa kama wanamilima wengine. Wao hunyonyeshwa sawa na watoto wengine wa Wanamilima. Wao hucheza sawa na watoto wa wanamilima.
“Nao wakijikwaa hutoa damu rangi moja na Wanamilima wengine. Damu yao ni nyekundu, si buluu, kijani kibichi au hudhurungi. Nao hulia sawa na Wanamilima.
« Anapotimia umri wa kuoa, zeruzeru hupenda kama Mwanamilima yeyote yule. Anaweza kuhisi upweke ambao mapenzi huukabili. Japo ngozi yake haina rangi, zeruzeru anaweza kubaini rangi ya mapenzi na kupenda. Na anajua sikitiko na kero za mapenzi. Wapo watakaompenda, wapo watakaoidharau penzi lake, wapo watakaomzuzua na penzi vuguvugu. Lakini zeruzeru aweza kupenda na kupendwa.
« Ni ngozi yake tu iliyo tofauti. Na Maulana ndiye amemfanya hivyo. Zeruzeru katu hakuzaliwa zeruzeru kwa hiari. Asilani! Ni sawa na wenzetu wanamilima wenye vilema. Naam, maumbile ya Mola haina doa na sisi Wanamilima hatutouliza maswali.
“Ndio maana siwaelewi Wanamilima tena. Ukatili umetuingia kama pepo mchafu. Utu tumekosa. Tumekuwa hayawani. Hata afadhali hayawani kwani hayawani hupenda na kujali.
“Vipi tuwatumie ndugu zetu zeruzeru kama kafara na tambiko za kiganga?
Vipi tuwauze sawa na vitu mnadani ilhali ni wanamilima wenzetu?
Zeruzeru walitufanya nini ili tuwaue na kuwaangamiza?
Kosa lao ni lipi kuzaliwa zeruzeru?

“Wanamilima wenzangu ikiwa kuna wachawi basi ni sisi. Ikiwa kuna wauaji basi ni sisi wanamilima. Twajigamba eti sisi tuna ustaarabu na stara ilhali tunawadhulumu zeruzeru wenzetu. Zeruzeru anapovaa kofia ili kujizuia dhidi ya miale mikali ya jua tunamcheka na kumwita mzungu mchafu. Watoto wetu tukawastahimili wanapowakejeli zeruzeru. Nafasi za kazi tukawapunja hata katika nyakati ambazo zeruzeru ana shahada na taaluma katika kazi husika. Mafuta za kujipaka ili kuzuia makali ya miale ya jua bado tukaitoza ushuru na kuwaangamiza zeruzeru katika lindi la mateso. Zeruzeru akawa kama mbwa koko, hapendeki. Sawa na mnyama akawa anawindwa, kuandamwa na kuwawa. Zeruzeru akawa ametengwa na jamii ya wanamilima sikitiko lake lisiweze kusikika.
Nasi wanamilima kila siku twahubiri kuhusu haki. Tutaonekana televisheni na majukwaa ya kifahari tukikashifu na kulaani unyanyasaji na dhuluma za kila aina katika jamii ya wanamilima. Lakini jioni katika giza zeruzeru atachinjwa ili kutibu ukimwi na kufukuza mapepo. Pasi na kuangaziwa, Robinson Simiyu atahadaiwa kufunga safari kwenda Tanzania kupata ajira ya kuwa utingo ili afanywe tambiko la kiganga. Robinson Simiyu hatumpi ajira nchini. Na kama taifa la wanafiki na mafarisayo na masadukayo tutapokea habari ya kunusuriwa kwake kama mshtuko. Tutamwelekeza Robinson Simiyu mbele ya kina Paparazi ili tujiimarishe kisiasa lakini sheria ya kumlinda hatutaipitisha. Wiki mbili zikiisha tutamsahau Robinson na zeruzeru wote. Tutajishughulisha na mambo mengine za kutukera . Zeruzeru wanaweza kuangamia na kwenda kuzimu!
Ah! Wanamilima! Siwaelewi tena! Naam, zeruzeru ataendelea na maisha yake. Waweza kumdharau, kumkejeli, kumfitini, kumkebehi. Waweza kumfanya tambiko la kishirikina. Waweza kumuandama na kumchinja. Lakini ukweli utasalia kuwa zeruzeru ni binadamu kama wewe.
Wanamilima, mmenisikia mimi na nyuso zenu zaonyesha kukerwa na tukio hili. Sihitaji kero zenu, sihitaji kusikitika kwenu. Huruma haisaidii. Twaweza kufanya nyoyo zetu ziwe ngumu au twaweza kuzifanya laini ili kujenga taifa moja ambalo zeruzeru hatabaguliwa na kudharauliwa. Taifa hilo la Wanamilima ni taifa twaweza kulijenga pamoja. Itaanza kwa kubadili fikra zetu dhidi ya ndugu zetu Wanamilima: Zeruzeru.

No comments:

Post a Comment