Mwana wa Milima, ninaandika barua hii nikiwa jela. Hata ingawa ninaiandika katika karatasi shasha, la mno ninalokutaka radhi liwe ni ujumbe ninaowasilisha. Yapo mengi ningetaka kukuambia lakini muda na barua hii haitoniruhusu, Mwana wa Milima.
Jela inasikitisha. Mara nyingi naona heri nijitie kitanzi juu ya paa; nife Maskini aliyedharauliwa na kuonewa kero. Mara nyingine mimi hujiona nikisimama mbele ya askari na kumwambia: “Elekeza mtutu wa bunduki kwangu, nifyatue risasi, lipua ubongo wangu utawanyike mara elfu”. Na mara nyingine mimi hujipata nikitafakari jinsi ambavyo kifo changu kitapokelewa. Wafitini, wadhabidhabina na mahasidi watarusha roho zao na kuitisha karamu. Labda kifo changu kitakuwa cha kawaida. Haitatangazwa redioni wala magazetini. Labda sitazikwa. Labda kipande cha ardhi kitakosekana kwani mimi ni fedheha.
Lakini Mwana wa Milima, nakuomba usome barua hii hadi mwisho. Baada ya hapo, maadamu ni karatasi shasha waweza kuitumia msalani. Waweza hata kunifokea na kukaripia nyendo zangu. Hilo halinipigi mshipa. Cha mno hivi sasa ni kuwasilisha ujumbe huu.
Usidanganywe, Mwana wa Milima, ukiulizwa ni kipi cha kukukata maini zaidi jibu si umasikini. Jibu si mali nyingi. Jibu si njaa wala shibe. Hata jibu si elimu. Waweza kuuliza: Ni ajabu hilo, ni falsafa ipi inayokuandama?
Hii si falsafa wala zoezi la kisosholojia. Abadan! Ni mdahalo nawe Mwana wa Milima. Na chilumbo hili labda laweza kuwa la mwisho. Maisha ya jela ni upepo. Leo upo, kesho haupo umekuwa Mwendazake na kipindupindu.
Ulipozaliwa, Mwana wa Milima, ulikuwa uchi. Lakini ulikuwa huru. Ulipoendelea na maisha yako, minyororo ikakuzunguka. Wengi hunicheka. Husema: Mfungwa Maskini Mungu Amrehemu. Lakini iwapo kuna watu wanaohitaji rehema mara kumi ni ninyi mnaojigamba mko huru.
Katika jela, nimezungukwa na kuta za binadamu. Nimegubikwa na giza na harufu mbaya ya kutisha. Ninyi msio jelani mwadhani hamjazungukwa na kuta zozote wala giza wala harufu mbaya. Mmekosea! Mimi jelani niko huru akilini. Timamu zangu zinapepea katika anga za juu za Mwewe na Shomoro. Ninafikiria na kuunda mambo akilini bila kejeli wala wasiwasi. Na woga wangu nimetundika mitini, haziniandami.
Na ninyi je? Akili zenu ni finyu. Mwaogopa kufikiria. Mwapenda vya bure na vya rahisi. Njia zenu ni za mkato. Lenu ni kuiga. Akili zenu mwaiga, mienendo zenu ni za kuiga, kuongea kwenu ni kwa kuiga, mapenzi yenu ni ya kuiga. Kuta zilizowazingira ninyi zashinda hizi za jela. Japo taa zinawamulika kotekote maisha yenu ni ya giza. Kila mnakoenda mna woga. Mwaogopa kila kitu. Mwaogopa binadamu, mwaogopa kifo ilhali mwataka kwenda mbinguni, mwaogopa kuishi. Ajabu ni kwamba ninyi mwajiona mko juu, mmefura kama kaimati.
Hii ndiyo maana, Mwana wa Milima, sipati tamaa ya maisha yenu. Mmebaki vikaragosi na wanasesere. Hata nife leo, Mwana wa Milima, niko radhi kuishi katika nyendo zangu na upeo wa akili zangu kuliko majisifu na majigambo yenu yasofaidi chochote. Hata nifyatuliwe risasi jelani nitabaki mimi.
Lakini usikonde Mwana wa Milima. Japo ngano zako zitabakia ngano tu, jipe moyo. Ari, Mwana wa Milima, ipo siku inshallah, ipo siku….
Wasalimie wote,
F.L.R
No comments:
Post a Comment