
[Picha kutoka kwa toptipsfortrips.blogspot.com]
First they came for the communists, and I didn't speak out because I wasn't a communist. Then they came for the trade unionists, and I didn't speak out because I wasn't a trade unionist. Then they came for the Jews, and I didn't speak out because I wasn't a Jew. Then they came for me and there was no one left to speak out for me- Pastor Martin Niemoller
Tafsiri:
Mwanzo waliwajia wakomunisti, nami sikuzungumza kwani sikuwa mkomunisti. Kisha wakawajia, nami sikuzungumza kwani sikuwa.Kisha wakawajia mayahudi, nami sikuzungumza kwani sikuwa myahudi. Kisha wakanijia mimi lakini hakukuwa wakunizungumzia kwani hakukuwa na yeyote. - Pastor Martin Niemoller
Tuambiane ukweli: tunapowachagua viongozi wetu kisha tukasikika tukiguna kuwa hawatuwakilishi sisi katika maeneo bunge yetu au hata kutamka maneno yasiyoandamana na imani na misukumo yetu ni nani wa kulaumiwa zaidi kama si sisi? Je, ni nani mwenye akili mauzauza iwapo kiongozi huyu hataoa sera zetu na maendeleo tunayotaraji kutoka kwake? Iwapo kiongozi huyu tutamtazama katika runinga akituhimiza kusikiliza porojo zake zisizo msingi, ni nani wa kulaumiwa?
Naam, wapo viongozi wanaojaribu kupalilia amani na maendeleo na kuirutubisha na semi zilizojaa heshima na falsafa zinazotupandisha ari ya kufanya vyema zaidi. Wapo viongozi ambao hulka zao pekee hazitowaruhusu kuipora mali yetu ya umma ili kujibinafsisha. Wapo viongozi ambao darahima si suala ambalo litawasukuma katika matamshi na matendo yao. La kuvunja moyo labda ni kwamba hawa viongozi ni adimu sana hapa nchini waweza kuzunguka Kenya nzima ukatamaushwa na uchache wao!
Wengi wa wanasiasa wetu wanahitaji maombi. Sikusudii kukushtua lakini ukifungulia runinga yako saa moja jioni utasikiza vitimbi vyao visivyo na msingi. Cheche za matusi wataziamsha, vichekesho visivyo na msingi wa kuendeleza udugu watavisema, propaganda watazua alimradi katika mitazamo yao itawaongezea “political mileage” si hoja. Mola turehemu.
Vipengele katika katiba vitafanyiwa kazi chapwa kwa kuguna au kwa wasiwasi ya mwasi. Katika bunge letu, miswada haitapitishwa na kujadiliwa ipasavyo bali vita vya ndani kwa ndani ya kujijenga kisiasa au kuharibu mwenzio kisiasa vitakuwa vitu vya kawaida na ya kukubalika. Nje ya bunge, tutawasikia wakitueleza jinsi ambavyo mdahalo ulinoga ilhali tukiwatazama katika runinga walikuwa wamesinzia.
Na sisi? Na sisi je? Tutasalia na shida zetu tu tusiwe na wa kutuhimiza au kututimizia malengo. Katika giza na simanzi ya vyumba vyetu tutalalama tusiwe na wa kutuhamasisha. Katika giza la usiku kama huu, tutatapatapa bila mwelekeo tusijue jinsi ambavyo siku ya jua ya maendeleo na sera za kujenga zinavyopendeza. Tutakapofumaniwa na ushirikina wa umaskini na kifo cha ghafla kwa ajili ya dhiki zinazotuandama, hakuna atakayesikiza kelele zetu za mayowe. Kelele zetu zitabaki kelele zetu tu na kero kwa viongozi wetu tuliowachagua. Si ajabu katika majumba yao ya kifahari watamaka:
“Vilio vyao vya pesa nane si muhimu! Ikiwa wanadhani watanitisha wajitose basi katika bahari waliwe na papa na nyangumi! Sauti zao zinaudhi, ni kelele katika masikio yangu!”
Kuna nukuu moja ambalo linanihimiza mno. Linasema, “taifa hupata viongozi ambao linachagua”. A nation gets the leaders it chooses. Ikiwa taifa litachagua viongozi ambao wataendeleza maadili na sera yake, taifa hilo litaendelea. Ikiwa taifa litachagua viongozi ambao ni wabadhirifu, wanaopenda upyoro, wanaoweza fanya lolote ili kunyakua viti vya kisiasa na wafisadi waliopora taifa letu, taifa hili litazidi kusalia nyuma kimaendeleo. Jukumu hili ni letu. Tuwachague viongozi wanaotupeleka mbele na si vikaragosi ambao misingi yao maishani ni kukusanya mihela na kuchemua matusi!